Swahili Tales/Mtu ayari na hamali
MTU AYARI NA HAMALI.
Mtu alikuwa ayari, huenda sokoni akinunua vitu, akiisha nunua wale watwekao hawapi ujira wao.
Siku moja akanunua sanduku ya bilauri, akatafuta mtu wa kumchukulia, akapata hamali akamwambia, katika mambo mawili khitari mojawapo, kukupa ujira wako, ao nitakupa maneno matatu ya kukufaa ulimwenguni. Akamwambia, mapesa napata killa siku, nitakuchukulia kwa haya maneno matatu, utakayoniambia.
Akachukua sanduku. Akipata thulúth ya njia akamwambia, bwana wangu, sanduku hili zito, limenilemea, nipe neno moja, nipate kupata afia za kuenenda.
Akamwambia, mtu akikwambia, utumwa bora kuliko ungwana, usimsadiki.
Akamwangalia sana, akamjua, huyu mwenyi sanduku hii ni ayari, lakini ni kheri nisubiri hatta nifike. Wakaenenda, wakipata thulúth ya pili, akamwambia, niambie neno la pili.
Akamwambia, mtu akikwambia, umasikini ni bora kuliko utajiri, usimsadiki.
[ 414 ]Wakaenenda hatta walipofika nyumbani. Akamwambia, bwana niambie neno la tatu. Akamwambia, tua. Akamwambia, nina furaha mno kwa yale maneno mawili ulioniambia, niambie la tatu, nipate kutua.
Akamwambia, mtu akikwambia, njaa ni bora kuliko shiba, usimsadiki.
Akamwambia, jitenge, bwana, nilitue. Akaliinua juu ya kitwa, akalipomosha. Mwenyewe akamwambia, a-a-a umenivunjia sanduku yangu!
Akamwambia, na mtu akikwambia, imesalia bilauri moja katika sanduku hii haikuvunjika, nawe usimsadiki.