Ee mwongo, mimi sitaki maneno yako leo, mimi nataka uniache tu, ukae na suria yako.
Marra pale akaja mtu, akamwita, Fundi! Ameitika, lebeka. Akamwambia, nna maneno matano nataka kukwambia. Akamwambia, Ee walla. Akamwambia, bassi njoo, tukanong'one. Akamwambia, Ee walla. Akamwambia, kuna mtu ataka mwanao kumoa. Akamwambia, vema mimi napenda sana. Akamwambia, wamwona ugomvi kwa nyumba hapa, mimi na mke wangu, kwa sababu ya kijana huyu nimemnunulia mtumwa, bassi mke wangu amenena ni suria yangu mimi, bassi afathali aolewe mwanangu, na mimi nipumzike. Akamwambia, na mimi nimekubali. Bassi akaenda kwenda kumjibu yule mwanamume anaoposa maneno aliojibiwa na babaye mchumba wake.
Hatta alipokwenda akamwita yule mwanamume anaoposa, akamkuta nyumbani amelala, akamwambia yule mtoto alioko nyumbani, mwamushe marra moja, amenituma maneno, nataka kumjibu majibu naliopewa huko ntokako. Akamwambia, Ee walla. Akaingia mtoto hatta ndani, akamwamusha, baba! Akaitika na'am, mbona uniamsha? Waniamushia nini, usingizi wangu haujaniisha? Akamwambia, ni tume wako, waliokomtuma amekuja kukujibu. Akanena, bashire kheiri. Akaondoka hatta nje. Akamkaribisha, Karibu, Je! habari za huko utokako. Akamwambia, huko njema, sijui wewe nafsi yako. Akamwambia, nafsi yangu nimetangulia kupenda, haikutangulia kuiza.
Akamwambia, nimetumwa na mkweo, Salaam nyingi, baada ya salaam, hapana zema walizomtenda kamazo.