Alipoona akalia sana. Akafanya matanga. Akashukuru Muungu.
Siku nyingi zimepita. Yule kijana mwanamke mwituni akamwambia rafiki yake nyoka, nataka kwenda zangu kwetu. Akamwambia, kamwage mama yangu na baba yangu, watakapokupa rukusa kwenda zako, wakikupa zawadi, usikubali ela pete ya baba na kijamanda cha mama.
Akaenda akawaaga, wakampa mali mengi, akakataa akawaambia, mimi mtu mmoja nitachukuaje mali haya? Wakamwambia, wataka nini? Akamwambia, weye, baba, nataka pete yako, na weye, mama, nataka kijamanda chako. Wakasikitika mno, wakamwuliza, aliokwambia nani habari hii? Akawaambia, mimi mwenyewe najua. Wakamwambia, hakuna, ni huyo nduguyo, aliokwambia.
Akatwaa pete, akampa, akamwambia, pete hii nakupa, ukitaka chakula, ukitaka nguo, ukitaka nyumba ya kulala, yambie pete, itakutolea, kwa rathi ya Muungu na mimi babayo. Na mamaye akampa kijamanda, akamwambia vile vile. Wakampa na rathi.
Akatoka, akaenda zake, hatta kule mjini kwa mumewe asifike nyumbani kwa mumewe. Akifika kiungani, akayambia pete, nataka utoe nyumba kubwa. Ikatoa nyumba, na pambo la nyumba, na watumwa. Akakaa kitako, yee na mwanawe. Na mwanawe amekuwa kijana mkubwa.
Mfalme akapata habari, kuwa nyumba kubwa kiungani, akatuma watu kuenda kutezama, wakamjibu, kweli. Akaondoka Sultani na mawaziri yake na kijana chake.