Alfán akamwambia Bolukia, sasa tufanye tundu ya kumtegea Sultani wa nyoka, akiisha ingia ndani ya tundu, tulifunge, tumchukue.
Akamwambia, haya. Akafanya tundu, akitia vikombe viwili, kimoja cha maziwa, kimoja cha mvinyo. Wakaenda hatta wakafika jabalini.
Nipo sijaondoka bado kwenda mjini kwangu. Wakaenda, wakaweka tundu ile, nikaingia ndani nikanywa mvinyo, nikanilevya, wakanifunga, wakanichukua.
Hatta nilipoamka, naona nimechukuliwa na watu, na yule Bolukia yuko ndiye alionichukua. Nikanena, waana Adamu si wema, wataka nini sasa? Wakaniambia, twataka dawa tupake miguuni mwetu, tukanyage bahari hatta tufike tunakotaka. Nikawaambia, twendeni.
Wakaenda nami hatta kisiwani, na kisiwa kile kina miti mingi. Na ile miti ikiniona hunena yote—mimi dawa ya fullani—mimi dawa ya fullani—mimi dawa ya kitwa—mimi dawa ya miguu—hatta ule mti ukasema, mimi, mtu akipaka miguuni hupita juu ya bahari.
Wakanena, ndio tutakao. Wakatwaa mwingi. Wakarudi, wakanipeleka hatta pale jabalini. Wakanifungua, wakaniachia. Wakaniambia, kua heri, nikawaambia, kuaherini.
Wakaenda zao, wakipata bahari hupaka miguuni, wakapita. Wakaenda vivyo hivyo hatta wakafika siku nyingi sana wakakaribia alipolala nabii Sulimani. Mahala karibu, Alfán akafanya madawa yake, wakaenenda.